Sunday, February 28, 2010

KARIBUNI KATIKA MAISHA YA NDOA MR & MRS GEORGE.

BI .  HARUSI - WINIFRIDA
BW. HARUSI - GEORGE
UKUMBI - HILL TECH (BANANA)
SALON - DOUBLE ''T'' HAIR DRESSING SALONWINIFRIDA

MR & MRS GEORGE

VIOLET AU MRS DENIS- Msimamizi waBi harusi

Mr. Denis -Msimamizi wa Bw. harusi


Hapa anatambulisha ndugu wa upande wake

tunapeleka keki ukweni - full unyenyekevu

zamu ya wao nao kupeleka keki ukweni

kila mtu akimlisha keki msimamizi wake - ishara ya upendo

it was fun kiukweli,

KILA LA KHERI WATOTO WETU, MWENYEZI MUNGU AWAJALIE YOTE YALIYO MEMA, NA AWAEPUSHIE YOTE YALIYO MABAYA JUU YENU

Friday, February 26, 2010

SIWEZI KUTULIA NA MWANAUME MMOJA - NISAIDIENI

Jamani, nina shida kubwa sana, ambayo hata sijui kama nitakuja kuepukana nayo, na kwakuwa mficha uchi hazai, nimeona niseme ili nisaidiwe, mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 27, nimezaliwa na kukulia UK, ambapo ndipo alipokuwepo mama yangu, baba alishafariki wala sikuwahi kumuona

nilipomaliza elimu ya secondary nilikuja tanzania kwa aunti zangu ambao tunaishi nao hapa Mwanza, Nilikaa kwa aunt zangu, wakati nikiwa kwenye process za kutaka kurudi kwa mama, bahati mbaya mama yangu alifariki, hivyo sikuweza kurudi tena kule, na kuamua kubaki tanzania kwa ndugu wa mama yangu

hapo nilikuwa ninamiaka  23, nilifanikiwa kupata kazi airport, nilifanya kwa muda wa mwaka mmoja tu, nikapata mchumba, ambae alinipenda sana, na aliahidi kunioa, basi nami nilimpenda sana, nilimtambulisha kwetu akajulikana, na kwao alinitambulisha, kabla ya kufunga ndoa nilipata ujauzito, ambapo familia yangu iliamua nizae ndipo nifunge ndoa, ikawa bahati mbaya, kabla yakujifungua nilipata kifafa cha mimba, hali ambayo ilisababisha mwanangu afariki,

nililia sana, tokea pale mchumba wangu akasafiri kwenda kusoma, na kudai nisubiri arudi ili tufunge ndoa, ajiandae vizuri, nilikubali, lakini aliposafiri tu! mawasiliano yalikufa, wakwe zangu wakaanza kunidharau, nikienda kwao nikama mzigo, hali hii ilinisumbua sana, kwakuwa nilimpenda sana mchumba wangu, nimekaa mwaka mmoja, nikapata taarifa kwa watu kuwa mchumba wangu anao, na vikao teyari,

niliumia sana, nakumbuka nilikunywa sumu kabia, mama mdogo aliniwahisha hospitali, nikapona, sasa tokea hapo, mimi sikuwa nikitaka mwanaume wa kunioa, wachumba walikuja niliwakataaa, nikawa kama niliechanganyikiwa vile, sasa hali ile hadi leo nikikumbuka, nalia sana,
TATIZO NI HILI,
niliamua kuwa na boyfriend, ambae nae tulidumu nae kidogo tu, akaniacha, baada ya muda mfupi nae akatangaza ndoa na mwanamke mwingine, hapo ndipo nilichoka kabisa,
niliwadharau wanaume wote, waliokuwa wakipita mbele yangu, nikawa nalala nao hovyo tu, hakuna niliempenda, akinitaka nikimtamani tu! nalala nae,  siku moja , ya pili nakuwa sihitaji kumuona kabisa, na simu yake naweza hata kudelete,
hadi sasa sijui nimefanya mapenzi na wanaume wangapi, NA SIWEZI KURUDIA KULALA MARA MBILI NA MWANAUME MMOJA, siwezi kabisa dada, yani kabla ya tendo lenyewe, nakuwa na hamu nae sana, nikimaliza tu! namchukia kupita kiasi,
dada, niko kama kahaba fulani hivi asijuwa muelekeo wake, yani napenda sana kufanya mapenzi na wanaume tofauti tofauti, sio mmoja, familia hadi imeamua kunitenga, maana ninayofanya ni uchafu sana, nimepoteza muelekeo wa maisha yangu, nikaamua kuja dar es salaam, nikapata kazi hapa ........... napo hadi sasa toka nije sijui nimetembea na wanaume wangapi, kila atakaenijaribu tu! nammaliza, niko teyari kufata mapenzi hata mikoani, nikishafanywa tu! narudi natulia,

kipindi cha mwanzo nilikuwa naona sawa tu, nilijitambua kama mimi ni malaya, sikuwa tayari kupima hata ukimwi maana nilijuwa ninao, lakini cha kushangaza, kuna siku niliumwa sana nikiwa geto kwangu, rafiki yangu alinishauri twende hsptl nilikataa kabisa, baada ya kuzidiwa sana, nikasema liwalo na liwe, nikapelekwa hospitali, katika vipimo walivyopima, damu yangu ikawa iko safi, sikuamini kabisa, hapo hapo niliona nimepona, nikawa na malaria tu!

baada ya miezi mitatu nilirudi kupima tena, nikakutwa safi, hadi sasa idadi ile ya wanaume imeshuka sana,
lakini mbona naona nateseka sana? nakuwa na hamu sana ya kufanya mapenzi, hadi naota kabisa nafanya mapenzi, hali hiii inanipa shida, sijui kama inatibika, natamani kuwa mtu mwenye heshima, natamani kurudisha heshima niliyoipoteza, natamani kurudi na kuanguka kwa ndugu zangu ili wanipokee upya, ila sijui kam nitaweza nimeshazowea, nisaidieni walimwengu.

Thursday, February 25, 2010

MSIONE NIMEDODA- MWENZENU NINA ''TEST'' CHUONI,

Kusoma ukubwani kazi kweli jamani, ah! ukirudi nyumbani shida tupu, tracy anataka kuandika nayeye, timo nae anataka umfundishe kusoma
mara mgeni huyu kaja unaitwa, mara usingizi, yani taflani tupu, basi muda wangu mwingi nasoma nikiwa kazini ninapopata kinafasi tu! basi mimi na daftari hivyo msione kimya sanaaaaaa mkajua nimedorola, namalizia test chuoni, then tutakuwa pamoja,

mlionitumia mikasa yenu, pia wala msikonde wapenzi wangu, tupo pamoja, nikimaliza test tu!  nairusha, iko mingi, na mirefu, so i hv to edit, msijisikie vibaya jamani, karibu namalizia then tutakwenda sawa.
nawapenda wooooooooote

Wednesday, February 24, 2010

NI KWANINI UNATOA HARUFU MBAYA MDOMONI? UNAIJUA SABABU?
Inapofikia kuzungumzia usafi/urembo wa mtu mmoja mmoja wengi wanasahau kinywa kama ni sahemu muhimu sana. Inatakiwa kujali sana kinywa wakati wote ili kisiweze kutoa hewa mbaya. Imetokea mara nyingi sana, mtu anatoa hewa mbaya akiongea au ukimsogelea. Utasikia watu wanaambiza "Mh yule kaka mdomo wake unanuka au yule dada mdomo wake unanuka". Sasa hii ni aibu kwa mtu ambae unaonekana msafi nadhifu nywere mpaka viatu.


Sasa basi sio kwamba hupigi mswaki vyema ingawa wakati mwingine ni kweli watu wanarashia rashia tu kusafisha kinywa, hawa si wengi. Ila kama unasafisha kinywa vyema asubuhi na jioni na bado kinywa kinatoa harufu (KINATEMA) basi fanya jambo hili mara kwa mara ukiwa kwenye kazi zako. Kunywa maji mara kwa mara. Tafadhari sana usinywe maji kama vile unakiu! aaah sio hivyo. Chukua chupa yako ya maji ama glasi weka mezani kwako ili uwe unakunywa funda moja kila baada ya muda fulani. Ukifanya hivyo itakusaidia sana kusafisha kinywa na kuzuia kinywa kutoa hewa chafu. Wengine wanapendelea sana kutafuna vitu kama ChewGum ni sawa lakini hii inakusababishia tabia ya kutafunatafuna wakati wote. na hewa chafu haitolewi kwa kutafuna BIG G kama wanavyofanya wengi, urembo kuanzia kinywani jamani, ndio inanoga, ukiongea mtu anaskia raha kukusikiliza, na hatamani umalize

kuna mtaalamu wa afya mmoja, niliwahi kumdadisi dadizi akashauri watu kutumia zaid maji ya kunywa kwa wingi, sio kwa ajili ya mdomo tu, lakini maji yana kazi nyinig mwilini, mwingine kwake maji ni kama kituo cha polisi,  maji yanaondoa chunusi usoni, na kazi nyingine nyingi sana, maji yanazuia kuumwa kichwa mara kwa mara. yanakutia nguvu, ndio maana hata ukiharisha ukienda hospitali, wanakutundikia maji kwanza. Nafikiri kunawataalam zaidi watatusaidia kwenye tatizo hili la kutoa harufu mbaya kinywani. Na pia watatupa mawazo namna ya kuondoa harufu mbaya zaidi ya hizo mbili nilizosema hapo juu. au hata wewe kama unajua dawa ya kutoa harufu, unaruhusiwa kutushaur zaidiFriday, February 19, 2010

WAZAZI WA MPENZI WANGU HAWANITAKI, WAKATI MTOTO WAO ANANIPENDA NA NIMEZAA NAE.

Habari dada violet, umri wangu ni miaka 30, nilikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kaka mwenye umri wa miaka 36, huyu kaka alikuwa na madhaifu mengi lakini nilimvumilia kwa kila hali, kutokana na kumvumilia magumu yake yote na tunajuana vilivyo tukaona bora tuoane, akawa anajiandaa kuleta barua, nami nikawambia wazazi wangu, chakushangaza yeye wazazi wake wakakataa kabisa hasa mama mama yake, akadai huwezi kumuoa huyo msichana, sababu hana elimu,
halafu tupo majirani, ila vikwazo vikawa vingi kiasi ambacho yule mchumba wangu alichanaganyikiwa sana. huyo kaka amemaliza chuo kikuu na mimi nilisomea usekretari baada ya kumaliza form 4,

tulipoona wamekataa tukashauliana na mpenzi wangu na tukatafuta njia nyingine, tukashauriana mi na mchumba nikabeba mimba, loh ndo tuliaharibu kabisa, ikawa uhasama juu ya uhasama, mchumba wangu akaitwa na wazazi wangu akaulizwa mambo mengi na yote akakubali, shughuli ikawa kwa wazazi wake,

wazazi wangu wakaenda kwa wazazi wa mwanaume, majibu waliyotoka nayo huko ilibidi wasinambie mana ningeweza kutoa hata hiyo mimba wakati huo mimba ina miez 7,ilikuwa mwaka 2008 mwezi wa kwanza, nikawaambia mniambie tu, siku moja mama wazazi wangu waliniita na kuniambia kuwa wazazi wa mwenzio wamesema hivi "kwanini ubebe mimba wakati wao hawakutaki?


kwa hiyo hiyo mimba si ya mtoto wao, tena marufuku kumshirikisha mtoto wetu kwenye huo ujauzito",na maneno mengi ya kejeli, nililia sana, niliumia sana sitaki hata kukumbuka, basi nikashukuru mungu lakini yule mchumba wangu hakuniacha kwa kweli alinipa matumizi yote mpaka nikajifungua mtoto wa kike.

walichohadhirika mtoto katoka kafanana na huyo mama mzazi wa mchumba. waliona aibu sana, mchumba wangu akawa anamtunza mtoto,vizuri tu, mtoto alipofikisha miezi saba, mchumba akaanza vituko, mara haleti hela mara ana mwanamke na huyo mwanamke ananipigia simu na kunitukana na kunitamkia maneno makali makali tu!

nilikuwa nakaa kwetu sina kazi wala nini, ndo nasubiri mpaka huyo mchumba alete hela. nikaona bora nitafute kazi, nikapata kazi wakati huo mtoto ana miezi 9, nikaanza kazi, nikashukuru mungu kazi nilipata nzuri, nikahama nyumbani nikaamua kupanga chumba changu, lakini motto wangu nilimwacha kwa mama yangu maana alisema anataka akae na mjuu wake
Nashukuru Mungu kwakuwa mtoto wangu anaafya nzuri tu, na nikaona huyu mzazi mwenzangu amepoteza malengo yote juu yang anafanya mambo yake kivyake na tangia muda ule tukawa hatuna mawasiliano ya karibu akijiskia kuleta matumizi anapeleka kwa mama. ila dada Violet mimi nilipenda na nilitaka sana awe mume wangu, si kwa sababu ya elimu au vipi,

hapa ndipo panaponipa shida, maana hadi sasa nimejikuta sioni mwanaume yoyote ambae nampenda kama yule, halafu naogopa kwa sababu wanaume wenyewe wamekuwa waongo wote nawaona wa tabia moja,

hadi sasa hatuna ule ukaribu kama mtu na mpenzi wake. nasema hivyo kwa sababu alikuja anataka turudiane na miadi kibao ya kushi pamoja moyo wangu unasita sana japo nampenda, sijui nifanyaje naombeni ushauri wenu? Je kama nikikubali kumrudia wazazi wake watanipenda?

WAPENDWA WANGU, JARIBUNI KUFUPISHA MIKASA YENU MNAYOITUMA

My dears, tujaribu kufupisha mikasa tunayoituma,
ni mirefu sana, tuandike yale mambo ya msingi tu yanayohitaji ushauri, ili isiwape wachangiaji shida na uvivu wa kuisoma, ukiandika ndefu sana unanipa hata mimi kazi kubwa ya kuedit, na nyie mliotuma mikasa yenu na bado sijairusha kwa ajili ya kushauriwa , msidhani sijaipata, nimeipata, ila iko mingi, sasa utaratibu wangu nikwamba, natuma mkasa mmoja mmoja, mtu anashauriwa cha kufanya, then napost mwingine, nikituma yote kwa pamoja, hainogi, itawapa uvivu wachangiaji kusoma, na huenda wasisome kabisa,
so msione nimewatenga, hapana tupo pamoja na tutashauriana tu!
WEEK END NJEMA.

Thursday, February 18, 2010

NAMTAMANI MUME WA MAREHEMU RAFIKI YANGU KIPENZI

Violet pole na kukutwika mizigo mikubwa,

Mimi ni mama wa miaka 42, sijawahi kuolewa, ila nilibahatika kuzaa mototo mmoja wa kiume, nilizaa nikiwa mdogo maana mwanangu sasa hivi anamiaka 25, yuko Swaziland anasoma,
Nina maisha mazuri tu!, nina nyumba zangu nne, tatu nimepangisha na moja ninaishi mwenyewe, nina daladala nne, nina mifugo ya kutosha, nina kila kitu, lakini sijabahatika kupata mwanaume na kunitamkia kunioa, toka usichana wangu hadi sasa, sina ulemavu wowote wa kiungo, ila nafikiri sikuwa nimeandikiwa kuolewa labda,

Nimelia sana, pesa ninazo nina kila kitu lakini nimekosa kitu cha muhimu sana katika maisha yangu, na sitaki kufa kabla sijakipata, Unavyoonekana violet ni binti mdogo bado, lakini kwakuwa toka nimefatilia mambo ya humu ktk blog yako, na ushauri unaotolewa na watu, naamini UKUBWA WA PUA SI WINGI WA KAMASI, nahitaji ushauri toka kwako na wengine pia,

Nilikuwa na rafiki yangu mpenzi, nilimpenda sana, yeye aliolewa na mume wake tulikuwa tukiheshimiana sna, na walikuwa family friend wangu, mtoto wake mkubwa wa kiume, ni rafiki wa mwanangu sana, na wanasoma wote switsland, bahati mbaya mwaka juzi rafiki yangu alifariki ghafla tu!, alilala kichwa kinauma, akanywa dawa ya maumivu ili assubuhi awahi hsptl, ikawa bahati mbaya hakuamka tena,


Akawa amepoteza maisha, nililia sana, wakati huo hata shemeji yangu sikuwa nimeanza kumtamani, siku zinavyozidi kwenda, najikuta nampenda sana Yule baba, nae ni mtu mzima, nikimtumia sms za kumsalimia, anarespond vizuri, muda mwingine simu yangu inakuwa na salio la kutosha tu, lakini namjaribu kumuomba aniwekee salio kidogo, anaweka muda huo huo na na ananipigia kuniuliza kama nimeipata, yani akipiga siku mimi huwa akili zote zinahama, natamani asikate hata simu,

Kuna siku nilijifanya gari zangu zote mbovu ili anipe gari lake, akaniletea hadi kwangu, nikachukuwa nikalijaza mafuta full tank, sikwenda kokote, jioni nililirudisha, badae usiku akanitumia sms asante kwakuniwekea mafuta, usiku mwema, nilitamani kulia, inamaana hajui kama nampenda, na yote ile ni kutaka anizowee?

Yani ni mtu mwenye heshima zake, nikimualika aje mahali dinner, anakuja anakula namsindikiza anaondoka, ss sielewi je, hajajuwa bado kama namtamani? Inafikia kipindi hata nikilala namuota kabisa, yani hii imenitokea kama mara nne hivi, naota niko nae, naota nampikia anakula, naota nimelala nae , naweza chukuwa simu kumpigia ikiita tu! Nakata maana nakuwa sina hata la kusema, umri wake yeye mkewe aliwahi kuniambia ni miaka 50 ambapo hadi sasa ana miaka 53, anafanya kazi kwenye wizara moja hapa Dar es salaam, anacheo kizuri tu.

Violet naombeni mnishauri, kuna siku nilikuwa nikiongea na mwanangu, tumezoeana nae sana, nay eye ndio kila kitu kwangu, maana sina mtoto mwingine, niliwahi kumuuliza je nikipata mume niolewe utajisikiaje? Mtoto alichukia sana na kuniambia mama, futa hayo mawazo, sitakusuport kwa kitu chochote, umri huo unataka nini mama? Kwani umekosa nini wewe hadi uolewe sasa hivi

Mimi sitaki uolewe mama, sitaki, nilimshangaa sana, lakini yeye ni mtoto, hajui mateso ninayopata mimi, nimeamini kwama kuolewa ni bahati ya mtu, unaweza kuwa mzuri wa kila kitu na usiolewe,

Sasa huyu baba mimi nimempenda, ila najiuliza, je nikimwambia akikubali, jamii itanielewaje? Maana watu wote walikuwa wanajua mimi ni rafiki wa mkewe, mwanangu atanielewaje? Maana wototo wetu pia ni marafiki wa kufa na kuzikana, lakini pia nikikaa kimya moyo unauma sana, naogopa asije kupata mawazo ya kuoa mtu mwingine

{Najua kuna baadhi ya watu watanishangaa, lakini ukweli ni kwamba, nimempenda sana huyu baba}.

Wednesday, February 17, 2010

NAJUTA KUPENDA, NA NASIKITIKA KWA USALITI ALIONIFANYIA MPENZI WANGU"(Hii ni ndefu kidogo, ila tumshauri mwenzetu)

Hellow Dada Violeth,

Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 24,Mpare, Mkristo na nina boyfriend wangu mwenye umri wa miaka 30,Mkinga,Mkristo.Tumekuwa wapenzi kwa muda wa miaka mitatu (3).Lakini toka Christmas mwaka jana tumekuwa na migongano katika mapenzi yetu, yeye amepanga chumba kimoja, kwakuwa tulikuwa tunapenda sana nilikuwa huru kwenda kwake muda wowote ule, na funguo ninazo,
 
kazi zake yeye sometimes anaingia shift ya usiku kwa hiyo unakuta mimi nikienda anakuwa hayupo, au tunapishana, lakini mara nyingi tulikuwa tukionana nae juma mosi na juma pili.
 
siku zinavyozidi kwenda ndio akawa anazidi kubadilika, hana furaha na mimi hata nikienda kwake, hapo anapoka kuna mama wa makamo, ambae ndie mama mwenye nyumba,ambae ametokea kunipenda, na huwa ananishauri nimwambie boyfriend wangu kama kweli ananipenda basi anitambulishe kwa kwao,
 
wakati ndio tunaanza urafiki mimi na yeye, hakuwa na kazi yeyote ile, alikua akiishi na kaka yake, ila hali sikuipenda, mimi nilijitahidi nikamtafutia kazi ambayo ndio anaifanya hadi sasa, na badae kumsihi ahame akae kwake,
 
lakini yote hayo mchumba wangu huyu hakuwa ameyaona, siku moja aliingiza msichana mmoja ambae ni BARMAID(mfanyakazi wa baa) akalala nae, asubh wakati yle dada anatoka akakutana na mama mwenye nyumba, yule dada alistuka na kurudi ndani, yulekwakuwa ananipenda, siku nilipoamua kwenda kwa ajili ya kumfanyia mpenzi wangu usafi, yule mama aliniita na kunieleza lile tukio, nililia sana, niliumia na niliondoka bila kuuliza
 
lakini nilishindwa kuvumilia kabisa, usiku nikapiga simu kwa boyfrienda wangu ana kumuuliza, akakataa akasema sio mpenzi wake isipokuwa alikwenda kufata pesa yake, sikumuamni, toka pale mapenzi yangu kwake yakawa yamepungua sana,

Christmas 2009, ilikuwa ni majira ya usiku nilipigiwa simu na mtu ambae simjui, ilikuwa ni sauti ya mwanamke aliyenitolea maneno machafu na kuniambia tutabanana hapo hapo,haijalishi mimi na huyu mpenzi wangu tunamahusiano kwa muda gani ila kama nitakuwa nae mchana basi na yeye zamu yake ni usiku.Nilihisi maini yananitoka,kwanza nikajiuliza ni yule dada barmaid ameamua kunitusi hivyo au ni mtu mwingine tu katumwa??

Kumbe ni dada mwingine tena, ambae nae pia ni barmaid!, nliishiwa nguvu na kujiona nipo utupu kwani yule dada alinieleza kila nilichokuwa nafanyana na mpenzi wangu ikionyesha kuwa alikuwa pia ni mpenzi wake.Hadi mara ya mwisho tulipoenda kumsalimu wifi yangu yule dada alikuwa anajua kila kilichokuwa kinaendelea.Na matusi mengine ya kashfa kama"Wewe unanuka,unajipendekeza kwa ndugu zake, mwenyewe anasema hana muda na wewe, ameshanipata mimi ninamridhisha, hujui mapenzi mshamba tu!na isitoshe hapa nilipo ameshanivalisha pete na ni mjamzito.Akidai kuwa mimba yake ina miezi miwili!

Dada Violet,  nilichanganyikiwa wala sikulala, nikaamua kumpigia simu boyfriend wangu tena kujuwa kama ni kweli, matokeo yake simu ilipokelewa na yule mwanamke na kunijibu kwa jeuri, Anti!mbona lakini unakuwa sio muelewa?naomba uniachie mpenzi wangu na hatutaki usumbufu saizi, hapa tulipo tunajazia VIUNGO vya mtoto wetu, kama MIGUU na VIDOLE"

nililia sana, hadi mama yangu alishtuka na kuja kunigongea, niliogopa kumueleza mama ukweli kwakuwa ana pressure, hivyo nilidanganya kuwa nimeota nimepata ajali, basi mama aliniombea na kwenda kulala,
toka pale nikaamua kumsahau, nakuanza maisha mapya, nilichokifanya ni kwenda kupima afya yangu tu!
na nikaamua kuendelea na masomo yangu tu!,

baada ya muda akaanza kunisumbua tena ili turudiane, nilliona kero nikabadili namba ya simu, lakini aliitafuta kwa marafiki zangu na kuendelea kunisumbua kwamba turudiane nae,

Nipo kwenye mawazo sana, kwakuwa nilimpenda sana huyu kaka, na mafanikio yake mengi yametokana na juhudi zangu, amenitenda yasiyostahili, sasa hivi ndio anataka nimrudie tena, naombeni mnishauri maana sijui hadi sasa nifanye nini. Saturday, February 13, 2010

Thursday, February 11, 2010

KINA MAMA TUSIWE BUSY SANA KIASI CHA KUACHIA MAHOUSEGIRL KAZI ZOTE!

Kweli tuko busy na kutafuta maisha (pesa), kiasi kwamba lazima uweke house maid nyumbani ili aangalie watoto wako na kukusaidia baadhi ya kazi pale unapokuwa haupo.
Lakini tunajisahau sana na kuacha kila kitu kwa house maid, yani wewe ukishaitwa bosi, basi ndio kila kitu afanye mfanyakazi wako, unakuta hata kutandika kitanda chako na mumeo housegirl ndio anaetandika, 
maana wewe ndio uko busy, lakini ubusy wako usizidi kipimo,
mahousemaid wengine mabosi wao wakiwa hawapo, wanafurahi sana, wanafanya vituko vya kila aina, ukirudi wananyweaaa, wanakuwa wadogo kama piriton! wewe hujiulizi ni kwanini?
mwingine akimaliza kutandika ndio anapumzika kabisa anasoma na vitabu chumbani kwako
bora anaesoma kitabu utasema hakina shida, mahouse maid wengi wanaingia katika vishawishi kutokana na position aliyopewa ndani ya nyumba yako,
house girl atenge chakula kwa baba, tena sio atenge dinning room
anapeleka hadi chumbani alipo mumeo, kweli hii si tunawatega waume zetu??
hapo mama uko busy, nyumbani mwenyewe umemuacha DADA, aangalie familia
mh!


.
sasa, hapa analaumiwa nani?? house girl ndio anakusaidia hadi kunywa au kula na mumeo tena chumbani kwako, unafikiri mumeo mawazo yake yatakuwa kwenye hicho kinywaji au chakula alichopelekewa??

umeona matokeo yake eeeeeeee, baba ameshategwa, MDADA nae ndio anawajibika
mwenyewe ukiulizwa watoto umewaacha nanani, bila hata aibu, nimewaacha na DADA
haya sasa DADA anaacha kulea watoto anamlea DAD
HAPATOSHI........

hadi uje ushtuke ni TOO LATE, kama ndio una kitoto unakiacha na dada, basi kinaona mambo mengi, lakini ndio hakiwezi kusema, kwanza hadi urudi labda kitakuwa kimeshasahau kila kitu! kinaangalia tu!
LAKINI NANI ANASABABISHA HAYA YATOKEE??
Kweli kuna baadhi ya wanaume ambao hawaoni kichaka.......... lakini pia kwa sehemu kubwa tunachangia sisi wenyewe kina mama, si kwamba tusifanye kazi zetu,
kazi tufanye, lakini na housegirl nae umpe majukumu yake, yasipitilize, chumbani kwako akutandikie kitanda labda uwe unaumwa huwezi hata kunyoosha shuka,  mwingine ukimpata mstaarabu atakwambia, mama leo baba kaniambia hivi, lakini wa hivyo wachache, wachache sana, wengi wanakuja macho miamoja, anasubiri ategwe tu! ategeke, sasa kama unaweza zuia asitegwe kwanini usizuie?
anza na mume wako, bwanaeee chakula , kinywaji, vyote viliwe dining room, ukitaka chumbani usubiri hadi mimi niwepo!, unakuta mtu unaacha hadi nguo za ndani za mumeo unamrundikia housegirl afuwe, sasa ni nani mama hapo?? hiii nimeiskia kwenye  familia nyingi sana
mtu analalamika tu! housegirl wangu yuko hivi, yuko vile, sikuhizi anakiburi, unajibu nayeye anajibu, anakujibu si anaona mko sawa nae, kwani una nini ulichomzidi, kama ni baba nae anamjuwa kuliko hata wewe! kama  chupi za baba nae anafua, kitanda kile unachoamka wewe nae analala, sasa mnapishana nini?
MPANGIE HOUSEGIRL WAKO MAJUKUMU, kwamba dada, hakuna kuingia chumbani kwangu wakati baba yako yupo huku, ikiwezekana hakuna kuingia kabisa awepo, au asiwepo,  chumba chako na watoto ni hiki, unakuwa umezuia kitu, umemnyima sheteni nafasi, mengine ya kumshawishi baba wewe unaayajua
NI KWELI YAPO, NA YANATOKEA, TUSIJISAHAU SANA JAMANI


Wednesday, February 10, 2010

BREAKING NEWS
Breaking news kutoka mahakama ya rufaa: Babu Seya, Papii Kocha waendelea kutumikia kifungo cha maisha baada ya mahakama kuthibitisha walishiriki katika kesi ya kubaka , Wakati Nguza Mbangu na Francis Nguza waachiwa huru na kurudi ushwahilini
Inatia huruma sana, inasikitisha sana, waototo wawili wameachiwa huru na kurudi uraiani
lakini Nguza na Mwanae Papii warudishwa gerezani kwa kilio kikubwa sana!
habari hii imenihuzunisha sana!
Tuesday, February 9, 2010

UNAIELEWAJE VALENTINE DAY

siku hiyo zawadi zinakuwa nyingi sana, zenye red tu!

Wewe unaielewaje siku hii ya Valentine,
 kuna wengi wetu tunajua tu kwamba ni siku ya wapendanao, mwingine anakanusha na kusema kila siku tunapendana, hii valentine ina maana ingine tu!, hebu tuwekane sawa hapa.

NI SIKU IPI ILIKUUMIZA SANA MAISHANI MWAKO NA USINGEPENDA ITOKEE TENA????MM SITASAHAU SIKU NESI ALIVYOMVIRIGA SHUKA MWANANGU WA KIUME AKIDHANI  AMEKUFA! KUMBE NI MZIMA!

MIMI  KWA UPANDE WANGU, siku ambayo sitaisahau maishani mwangu ni siku ambayo nesi alifikiri mwanangu amekufa na kumviriga katika shuka ili mchukuwa mait akija amchukuwe na yeye, aisee, siku ile hadi leo nikikumbuka huwa moyo unaniuma sana, nina watoto wangu wawili (TWINS) baada ya kujifungua niliruhusiwa kwenda nyumbani, nikaka wiki moja waototo wakaanza kuumwa nikawarudisha tena hospitali,(Muhimbili)  nikalazwa, basi kama ilivyokawaida mtoto mchanga akilazwa, wanalazwa kwenye ward yao nyie wazazi kazi yenu kwenda kunyonyesha tu! kila baada ya masaa matatu,

basi mwenyewe ndio wanangu wa kwanza hao tena mapacha, wa kike na wakiume, niliwapenda kama roho yangu, baada ya siku mbili kupita mwanangu wa kiume hali yake ilikuwa mbaya zaidi, akawekewa oxgen kwa ajili ya kumsadia kupumua, nilipoendakunyonyesha mida ya saa sita, hali yake haikuwa shwari kabisa, lakini huwa namwamini Mungu sana, nilikazana kuomba na kumwambia Mungu, niachie watoto wangu? lakini kama ni mapenzi yako basi na yatimizwe ! Ilifika kipindi nikawa nalia tu! 

Baada ya kwenda saa tisa tena kunyonyesha, sikumkuta mwanangu kitandani, nilimkuta mmoja tu! yule wa kike ambae nae alikuwa anaumwa, nikauliza wenzangu walioanza kuingia, jamani mwanangu yuko wapi? mmoja wao akanionyesha chini ya kitanda, na kusema bahati mbaya!, amekufa!  nilijikuta naishiwa nguvu na kuanguka chini huku nikilia sana na kwa sauti, basi wakaja wakanishika wakati wananitoa nje tuko mlangoni tukakutana na Dr. mmoja mlangoni, akauliza nini? na kwanini kama mtoto wake amefariki mmemruhusu kuingia huku? wakamwambia kuwa nina watoto wawili, hivyo niliruhusiwa kuingia ili nikanyonyeshe aliebaki

Mungu wa ajabu jamani, yule Dr. akaingia hadi ndani na kuuliza yuko wapi aliekufa, wakamwonyesha, akamfungua shuka, kukuta katoto kanahema ila kwa mbaaaali kabisa, alicho kifanya na sitasahau alisema hivi
FUTA MACHOZI YAKO! MUOMBE MUNGU MTOTO WAKO NI MZIMA NGOJA NIMSHUHURIKIE, NISIKUSIKIE UNALIA HATA KIDOGO!, nilipata nguvu za ghafla nikasimama nikamfata Dk. nikamuangalia alichokuwa akifanya, alimuingiza mtoto puani mpira, akawa anamjaza hewa, gafla tumbo la mtoto likawa kubwaaaaa, akatoa ule mpira akamchukuwa mtoto wangu hadi kitandani akamuewekea mpira mwingine mdogo wa oxgen na kuniambia kila nikiingia kunyonyesha nihakikishe mpira uko pale pale puani, kisha akamuita yule nesi aliekuwa zamu na kuondoka nae, ambae sielewi ni action gani ilichukukuliwa juu yake, maana hadi naruhusiwa hospitali sikumtia machoni tena,

Kumbe pale alipokuwa amewekwa mwanzoni ni kwamba alikuwa akisubiriwa mchukuwa maiti aje azikusanye, hatimaye mwanangu aakawa mzima, huwa nikimuangalia simmmalizi, Mungu alinitetea sana, na nilisimama katika imani tu! nilikaa muhimbili  mwezi mzima, lakini MUNGU WANGU NI MWAMINIFU hadi leo wanangu ni wazima kabisa, na nikiwaangali tu! huwa nafurahi sana, nawapenda mno,  na siku ileile nilimsamehe yule nesi,

NA HAWA NDIO TWINS WANGU, TRACY & TYMON  ni wazima kabisa
na hapo walipiga mwaka jana mwezi wa tatu walikuwa wanatimiza miaka mitatu,
wamesheaanza kusoma, basi huyo mtoto wa kiume nikimuangalia, Mh! namshukuru Mungu tu!


Monday, February 8, 2010

MUME WANGU HANA HAMU NA MIMI- SIMUELEWI

nahitaji msaada wenu jamani
mume wangu hana hamu namimi kabisa, nakuwa nashindwa kumuelewa kabisa, yani huwa najitahidi sana kuwa karibu nae, huwa naonyesha kabisa kuwa namuhitaji na sio kunyesha tu! bali huwa namuhitaji toka moyoni kikweli kabisa, lakini mwenzangu huwa haonyeshi kabisa kama yuko namimi, mara nyingi sana imetokea hii, na kabla hatujafunga ndoa hakuwa hivi, kilichozidi sana ni pombe anazo kunywa, alikuwa akinywa toka zamani, lakini hivi karibuni amekuwa mlevi wa kupindukia, akirudi nyumbani ni kuanzia saa tano usiku, napo amelewa sana, 
 
alishawahi kupata ajali shauri ya ulevi, aliumia sana, Lakini Mungu alimsadia akapona ,alilpunguza kidogo kunywa pombe, baada ya muda akarudi kule kule, mbaya zaidi akaanza kunifundisha na mimi, mimi sikupenda kabisa maana sikuona wala kuhisi utamu, nikaacha wala sikuendelea kujifunza,
unakuta akirudi kama hajalewa sana basi anakuwa busy na shughuri zake zingine tu, ataangalia Tv hadi usiku sana, au ataanza kucheza game, yani hana hamu na mimi kabisa,
sikuwahi kusikia kuwa labda ana mwanamke mwingine, ila kwa jinsi alivyo sasa naanza kuhisi hivyo, ila nahisi vitu viwili, kama sio mwanamke mwingine, basi nahisi ni pombe anazokunywa.
kuna siku aliporudi nilimwambia kuwa namuhitaji, maana tulikuwa teyari tumefika wiki tatu bila kufanya kitu chcohote kile, siku hiyo aliwahi kurudi kwakuwa nilimdanganya mtoto wetu anaumwa, akarudi saa mbili, alipokuta mtoto mzima nilimuita chumani nikamwambia shida yangu, nikamueleza kwanini ananitesa hivi,
akauliza kwani nakupiga, au sikupi hela ya kula? nikamwambia hata kuwa mbali na wewe ni mateso kwangu,
akanifokea sana kwanini nimesingizia mtoto anaumwa na kunipa baadhi ya mifano kwamba inaweza kutokea kweli akaumwa, niliomba msamaha na kumwambia sitarudia tena ila kwa usiku huo anipe haki yangu, nilikuwa nikimuitaji sana, cha ajabu wala hakujali hisia zangu, ndio kwanza akapanda kitandani tena siku hiyo hakuoga wala kula, akalala, nikamwambia nimekuandalia chakula kizuri akasema anajisikia kuumwa nimuache apumzike, nilisononeka sana, kesho yake nikamdamsha ili twende hospitali akasema atanda mwenyewe, imefika usiku karudi kalewa sana, namuuliza kama alienda hospitali akasema alikunywa panadol akapona kabisa, sasa mimi sielewi jamani,
hali hii inanitesa sana mimi, niliwahi kumuita best man wetu na aliongea nae namimi nikiwepo, akatubu na kuahidi kubadilika, basi siku mshenga alipoondoka niliinjoy sana, kwani nilipata kile nilichokuwa nakihitaji kwa nafasi, niliona kama nimepelekwa mahali pazuri sana, nilijua hali ile itaendelea,
baada ya wiki kama mbili kupita, ikarudia pale pale, yani kumkuta nyumbani, hadi uweke apoint ment, hadi weekend yeye ni safari tu! hajui kanisa wala msikiti, tangu tutoke kushukuru kanisani ni baada ya harusi hakwenda tena, siku ya ubatizo wa mtoto alikwenda tena baada ya kumsema sana maana alisema yeye hatoenda, since that day, hajaenda hadi leo.

Dada violet, ananipa wakati mgumu sana mume wangu, kujali familia yake anatujali sana, tunakula, anampenda mtoto sana, hanipigi, ila hivi vitendo ambavyo anafanya simuelewi? je pombe imemaliza hamu yake??? kuna mwanaume kweli ambae ni kamili akaacha kumpa haki mkewe kwa takribani wiki tatu? nimempekuwa na kumpeleleza sana labda ana mwanamke mwingine, anasema hana, sasa mbona hanitamani??mbona haonyeshi kama anahamu namimi, mimi ni mzuri, najijuwa kabisa hilo halina ubishi, nimeridhika na mungu alivyoniumba. ninajiheshimu sana.
ananifanya nitamani sana ndoa za wenzangu, ananifanya nitamani hata kuwa na mwanaume mwingine ambae atautambua uthamani wangu, lakini naogopa sana, maana maradhi ni mengi, pia namuogopa sana Mungu,
unakuta hadi napoteza hamu yakula. na siku nikibahatika kula nae basi huwa nakula hadi najishangaa, nafurahi siku nzima, ila ujuwe siku akishinda nyumani anaumwa.hii imekuwa too much maana hata wazazi wake wakija anakuwa hivyo hivyo kunasiku alikuja mama yake mzazi kutusalimia, nikafurahi nikajua siku hiyo atawahi kurudi, lakini alirudi saa 6 na kukuta mama amekwisha lala, nilimsema sana, akalala bila hata kuoga, asubuhi akataka kutoka bila hata kumsalimia mama, nikafata nikamuuliza huyu ni mama yako mzazi au wa kukulea tu! akajitetea eti anaogopa kumsumbua nimuache alale, nikamvuta hadi kwa mama yake ndio kwa aibu akaenda kumsalimia, nilimuweka mama wazi,juu ya hali ile, mama alichukia sana alimsubiri hadi aliporudi na alimsema sana, akamwambia kama ananiona kero aniache nirudi kwetu asinifanye mlinzi, maana alikuwa hataki hata nifanye kazi anataka nikae nyumbani tu!
kama kawaida yake, aliomba msamaha tena, tukaka siku mbili hali ikarudi pale pele, nikitafuta mtu mwanaume mwingine nitakuwa nimekosea sana, sasa nifanyaje jamani?
ushauri wenu ni wamuhimu sana kwangu

Friday, February 5, 2010

Mazoezi ni Muhimu sana Kwa Afya Njema ( Weekend Njema)

Hii sijapata uhakika na vielelezo vya kutosha ila nilipata kusikia kwenye mazungumzo fulani mahali, kulikuwa na mkusanyiko wa wasomi wa mambo ya afya. Moja ya jambo ambalo walinigusa sana kwenye mazungumzo yale ni hili: Ajali kweli zinatokea kwa uzembe wa waendesha vyombo hivyo hasa hapa miji. Unakuta gari imepata ajali si mbaya sana lakini waliopoteza maisha ni wengi na ukiwachunguza hawana majelaha makubwa nje wala ndani ya mwili. Walisema sababu kubwa watu ni wazembe na ni twipwatipwa, utipwa tipwa sio lazima uwe kiiiibooonge sana. Hata huo mwili ulionao unawezakuwa tipwatipwa kuwa hauna mazoezi. Sasa basi unapopata mshituko mkubwa unakuwa hauwezi kuhimili vishindo hivyo na kukusababishia BP ya ghafla na kupoteza maisha. Kwa kifupi niliona kuwa mazoezi ni mhuimu kwa afya iliyo bora na si bora kunenepa tu.
Weekend hii naomba uanze mazoezi hasa wakati wa jioni unarudi nyumbani, fanya jambo lifuatalo. Shuka vituo vi3 kama viko karibu karibu au 2 ama 1 kabla ya kile unachoshuka kwenda nyumbani mwako kama unatumia daladala. Tembea kwa mwendo wa kasi mpaka ujisikie umechemka na jasho linakutoka, ukifika nyumbani utakuwa ushafanya mazoezi makubwa sana. Fanya hivyo kila siku utokapo kazini.
MAHITAJI:
1. Hakikisha unakuwa na SkinTYT ili kuzuia michubuko kwenye mapaja
2. Maji Masafi yasiyo ya baridi ya kunywa
3 Viatu Simple, ukipenda vile vinaitwa vibajaji
4 Leso ya taulo 100% Cotton ( Hii kwa wale wenye tatizo la chunusi inasaidia sana kutoa mafuta kwenye uso na kuuacha mkavu)

 FAIDA ZAKE:
1 Kuondoa uwezekano wa BP
2 Kujenga na kusafisha ngozi kwa kutoa jasho
3 Kuwa kakamavu (Strong)
4 Tabia ya mazoezi
5 Kutoka jasho usoni na kufuta kwa Taulo inasaidida kutoa mafuta yanayojihifadh kwenye ngozi ya uso na kukuleta chunusi.
6 Kupunguza uzito NK....
Data Fulani Kutoka Mtandao: IRISH MEDICAL TIMES